Idara ya Afya ilianzishwa rasmi mwaka 1990 na Mhas- hamu Askofu Antoni Mayala kwa nia ya kuratibu na kuimarisha shughuli zote za afya katika Jimbo Kuu la Mwanza. Shughuli za afya zipo katika nyanja za Kinga, Tiba na Mafunzo ambapo Jimbo Kuu lina hospitali mbili ya Bukumbi iliyoko wilaya ya Misungwi na Sumve (Hospitali Teule) katika wilaya ya Kwimba. Pia Jimbo Kuu linazo zahanati tatu ambazo ni Buhingo, Nyakahoja na Nyegezi na Kituo cha Afya kimoja cha Kagunguli, wilaya ya Ukerewe.
Upande wa Kinga Idara ya Afya ina miradi ya Afya ya Msingi ya Jamii, Mradi wa kudhibiti Ukimwi na mradi wa kuzuia Upofu. Idara ina vyuo viwili vinavyotoa mafunzo ya Uuguzi na Ukunga katika ngazi ya cheti ambavyo ni Bukumbi na Sumve.
Shughuli za Idara ya Afya
1. kuratibu, kutekeleza na kutathmini shughuli zote zinazohusiana na Afya katika Jimbo Kuu la Mwanza.
2. kuwa kiungo kati ya Jimbo na Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali na wahisani.
3. Idara inawajibika kwa Bodi ya Afya ya Jimbo katika maswala yote ya sera na utekelezaji.
Shughuli za kichungaji
Huduma za Afya zinatolewa kulingana na muundo wa Kansia ambao unaanzia ngazi ya Taifa hadi kwenye jumuiya ndogondogo za kikristo. Idara ya Afya inaamini ya kuwa inaendeleza tu kazi ambayo Yesu Kristo aliianzisha. Ni jukumu la kila mbatizwa kuhudumia wagonjwa.
Kwa kuona umuhimu wa Afya ya Roho, kila hospitali ina padre (chaplain) anayeshughulikia huduma za wagonjwa na wafanyakazi kiroho. Hata pale ambapo hakuna padre, bado huduma hizo hutolewa na wahudumu wengine wa Kanisa.
Huduma za Idara ya Afya zinatolewa kulingana na Maadili ya Kikatoliki ya Uganga (Catholic Medical Ethics).
Uongozi
Idara ipo chini ya uongozi kama ifuatavyo:
Mkurugenzi: Pd. Petro Chaha
Katibu Mtendaji: Dk. Raphael Mome